KOCHA wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameweka wazi kuwa msanii wa Bongo Fleva nchini, Ally Salehe Kiba ‘Alikiba’ ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza Ligi Kuu Bara, na kama akiandaliwa vizuri anaweza kucheza hata Ulaya.
Julio ameyasema hayo akiwa kocha wa Team Samatta mara baada ya kumalizika kwa mchezo maalum wa kuchangia elimu ulioandaliwa na msanii huyo akishirikiana na Mbwana Samatta anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya Genk nchini Ubelgiji. Katika mchezo huo uliopigwa juzi Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar, Team Samatta iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Team Kiba.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Julio alisema msanii huyo ni mchezaji mzuri na amekuwa akimwambia kuwa yupo tayari kumsajili achezee katika timu yake kutokana na uwezo mkubwa alionao na kama akiwekwa vizuri ana uwezo wa kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
“Alikiba ni mchezaji mzuri sana, mimi binafsi huwa namwambia ‘nataka nikusajili’, kama hawezi kuja kule mkoani lakini tukija hapa Dar aje acheze, ana uwezo mkubwa sana kuliko wachezaji wengi wa Simba na Yanga ambao wanalipwa mishahara ya bure.
“Isipokuwa tu nchi yetu haitaki kujua watu wenye uwezo, tunafuata majina na labda wana sababu zao, ndiyo hivyo lakini Kiba kama anatengenezwa hakuna ambaye anaweza kusema kuwa Kiba siyo mchezaji na kwa uwezo wake kama anacheza basi hapa atacheza ligi hii, mwaka wake mmoja tu anakwenda kucheza soka la kulipwa,” alisema Julio.
No comments:
Post a Comment