Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa kudownload APP YETU BOFYA HAPA, Au ingia playstore tafuta KALAMBO NEWS kisha bofya install.
MLIMA mrefu zaidi barani Afrika, Mlima Kilimanjaro, na Mlima Kenya unaoshika nafasi ya pili kwa Afrika, ni miongoni mwa milima mitatu inayotajwa kuwa hatarini kimazingira.
Ripoti iliyotoka hivi karibuni, inaelezea picha za setilaiti zikionesha milima mitatu iliyopo Kenya na Tanzania, ikionekana kama ‘visiwa’ kwa maana ya kwamba sehemu ya milima hiyo ndio yenye uoto wa asili, huku maeneo ya chini ya milima hiyo ikiwa imepoteza rangi yake ya asili ya kijani.
Shughuli za kibinadamu, hasa kilimo, ufugaji, biashara, viwanda na makazi zinaelezewa kuigeuza milima mitatu mikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, kuwa visiwa vya kijani katikati ya maeneo yaliyogeuka rangi kuwa njano au hudhurungi kwa mujibu wa picha za setilaiti.
Ripoti hiyo mpya ya kisayansi, inaonesha kuwa Mlima Meru ulioko Arusha ambao ndio wa pili kwa urefu nchini Tanzania, pia umekumbwa na adha hiyo, iliyougeuza nao kuwa kisiwa cha kijani katikati ya eneo linalogeuka jangwa kutokana na uvamizi wa watu.
Watafiti, Dk Andreas Hemp na Claudia Hemp wameandika katika ripoti yao kuwa, awali milima hiyo mitatu, maarufu na muhimu kwa ikolojia ya Afrika Mashariki, ilikuwa imezungukwa na uoto wa asili, lakini sasa, uoto huo umebaki kwenye miinuko ya milima hiyo tu, huku maeneo ya chini yakiwa yamevamiwa na watu, wanaovuna miti na kubadilisha mazingira hayo kuwa mashamba, viwanda na makazi.
Wanabaolojia kutoka Chuo Kikuu cha Bayreuth cha Frankfurt, Ujerumani ambacho pia ni Kituo cha Utafiti wa Mabadiliko ya Tabia Nchi, wamechunguza athari za viumbehai waliokuwa wanazunguka milima hiyo.
Wamegundua kuwa wadudu aina ya panzi na senene, ambao awali walipatikana maeneo ya chini kuzunguka milima ya Meru na Kilimanjaro, sasa wamehamia maeneo ya juu zaidi, katika kile kinachoelezwa kuwa ni kuwakimbia wavamizi wa maeneo hayo.
Nchini Kenya, tayari taasisi maalumu ya kushughulikia suala la uharibifu wa mazingira katika Mlima Kenya, imeanza kazi chini ya mkurugenzi wake, Susie Weeks ambaye anasema kuwa uvunaji wa miti ya mbao, kilimo na ufugaji, sio tu umeharibu uoto wa asili kuzunguka mlima huo, bali asilimia kubwa ya mito iliyokuwa ikitiririsha maji kutoka mlimani, nayo imekauka.
prop
Wednesday, 21 March 2018
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment