Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa kudownload APP YETU BOFYA HAPA, Au ingia playstore tafuta KALAMBO NEWS kisha bofya install.
MSICHANA mwenye umri wa miaka 14, amejisalimisha mwenyewe katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa akipingauamuzi wa wazazi wake wa kumuozesha kwa nguvu kwa mzee mwenye umri wa miaka 75, Mtokambali Chele, badala yake anataka apelekwe shule aanze kusoma.
Taarifa za uhakika kutoka eneo la tukio, zinaeleza kuwa baba mzazi wa msichana huyo, Matembezi Mugo, inadaiwa awali alimuozesha dada ya msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 kwa Mzee Chele, lakini alifanikiwa kutoroka kwa mumewe huyo baada ya kubaini kuwa kumbe ni mzee sana. Aidha, msichana huyo alibaini kuwa mume wake huyo alikuwa na wake wengine wanne waliomzalia watoto ambao idadi yao inakadiriwa kuwa zaidi ya 50.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, George Kyando alithibitisha kutokea kwa mkasa huo, na kufafanua kuwa msichana huyo alijisalimisha kituoni hapo wiki iliyopita akipinga uamuzi wa wazazi wake kumuozesha kwa nguvu kwa mzee huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Swaila wilayani Nkasi. Akisimulia alisema mzazi wa kiume wa msichana huyo, mwishoni mwa mwaka jana alimuozesha binti yake mwenye umri wa miaka 16 kwa Mzee Chele ambaye tayari alikuwa na wake wanne na watoto wanaokadiriwa kufikia 50 na idadi isiyojulikana ya wajukuu na vitukuu.
Majirani wa Mugo ambao kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini, walilieleza gazeti hili kwa nyakati tofauti kuwa kuwa alimuozesha binti yake huyo mwenye umri wa miaka 16 kwa mahari ya ng’ombe 50. Wanadai kuwa mke wa kwanza wa Mzee Chele ana watoto 14, wa pili ana watoto 13, watatu ana watoto 12 na wanne ana watoto 11. “Msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 ambaye ni dada yake na huyo msichana mwenye umri wa miaka 14 alipofikishwa nyumbani kwa “mumewe” (Chele) alibaini kuwa ni mzee sana isitoshe tayari alikuwa na wake wanne na watoto wengi tu ...akaamua kutoroka na kukimbilia kusikojulikana,” alieleza Kamanda Kyando.
Aliongeza kuwa baada ya msichana huyo kutoroka nyumbani kwa ‘mumewe’ huyo kijijini Swaila, Mzee Chele alimwendea baba mzazi wa msichana huyo na kumtaka amrejeshe mahari yake yote kwa kuwa binti yake ametoroka nyumbani kwake. “Ndipo Mzee Mugo alipomtuliza mzee mwenzake Chele kuwa atampatia binti mwingine ambaye ndiyo huyu mwenyewe miaka 14 akazibe pengo la dada yake aliloliacha nyumbani kwa Mzee Chele baada ya kutoroka... hakuwa tayari kurejesha mahari,” alieleza Kamanda Kyando. Aliongeza kuwa kwa usalama wa binti huyo aliyejisalimisha katika Kituo cha Polisi ambako sasa anahifadhiwa kwa muda na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Wilaya ya Nkasi, Anna Kisimba nyumbani kwake. Kutokana na mkasa huo, Kamanda Kyando alithibitisha kuwa tayari Mzee Chele ameshakamatwa.
prop
Sunday, 18 March 2018
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment