BEKI Mtanzania, Abdi Banda, anayecheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini katika Klabu ya Baroka, ameitaja sababu kubwa ambayo imesababisha Simba na Yanga kuondoshwa kwenye michuano ya kimataifa ambayo walikuwa wanashiriki.
Banda aliyasema hayo jana Jumapili alipotembelea Ofisi za Championi zilizopo Sinza Mori jijini Dar. Kwa sasa Banda yupo Tanzania baada ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Algeria na DR Congo.
Simba na Yanga kwa nyakati tofauti, juzi Jumamosi zilijikuta zikitupwa nje ya michuano ya kimataifa ambapo Yanga imeondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba kuondoshwa Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hizo zote zilitolewa zikiwa ugenini zilipokwenda kucheza mechi za marudiano ambapo Yanga walifungwa mabao 2-1 na Township Rollers kwenye mechi ya hapa nyumbani kisha wakatoka suluhu ugenini.
Simba wenyewe waliruhusu sare ya mabao 2-2 nyumbani na Al Masry ya Misri kisha wakatoka suluhu wakiwa kwenye mechi ya ugenini.
Beki huyo ambaye kikosi chake kinashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL), amesema kwamba timu hizo zimeshindwa kwenda mbele kutokana na kushindwa kutumia vyema viwanja vya nyumbani.
“Kilichozikwamisha timu za Simba na Yanga kwenda mbele katika michuano hii ya kimataifa ni kwa sababu wameshindwa kupata matokeo mazuri katika michezo yao ya nyumbani.
“Unajua kwenye mechi hizi za kimataifa ni lazima ufanye vizuri katika michezo yako ya nyumbani, sasa ukiwaangalia wao hawakufanya hivyo wakiwa nyumbani na kujikuta wakitupwa nje kwenye mashindano hayo.
“Lakini pia kinachokwamisha timu hizi zishindwe kwenda mbele ni kasumba ya mashabiki kushangilia timu za nje zinapokuja hapa nchini suala ambalo linachangia timu kushindwa kupata matokeo mazuri, jambo ambalo kwa sasa linatakiwa liachwe,” alisema Banda.
No comments:
Post a Comment