Mabalozi wa nchi za Kiafrika katika Umoja wa Afrika (AU) wako mjini Kigali Rwanda kuandaa makubaliano ya kuanzisha soko huria katika bara hilo.
Mabalozi hao wanasema kusainiwa kwa makubaliano hayo ni hatua muhimu kuelekea azimio la umoja wa Afrika la kuwa na soko huru lenye kurahisisha uendeshaji biashara.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti Jumapili kuwa ni makubaliano ambayo yanatazamiwa kusainiwa na marais 26 wa bara la Afrika wanaotarajiwa kukutana Kigali Machi 21, 2018.
Marais hao na wakuu wa serikali watakutana Kigali kwenye kikao cha dharura ambacho kinanuia kuanzisha mkakati huo ambao kimsingi ni mwanzo wa azimio la pamoja la kuwa na soko huria kwenye bara zima la Afrika.
Ni hatua ambayo waafrika wamekuwa wakiisubiri kwa hamu lakini balozi wa Rwanda katika AU ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya utendaji ya mabalozi hao, Hope Tumukunde anasema hii ni hatua ya kupongezwa na kwamba mataifa yapo tayari.
"Marais wetu watakuja wakiwa wamejiandaa kusaini makubaliano haya kwa sababu ni azimio ambalo walishaliazimia tangu mwanzo. Hii ni historia ambayo sasa inakwenda kuandikwa hasa baada ya wao kuweka saini makubaliano hayo. Wataionyesha dunia kuwa hii ni hatua ya mwanzo muhimu kwa bara la Afrika kuelekea muungano wa kweli," amesema balozi.
Kumekuwepo malalamiko ya muda mrefu kuhusu mataifa ya Kiafrika kushindwa kufanya biashara na uwekezaji miongoni mwao kama ambavyo yanafanya mataifa ya mabara mengine kutokana na vizingiti mbalimbali.
Lakini moja ya suluhu ya tatizo hilo ni kusainiwa kwa makubaliano haya ambayo yatatoa nafasi kwa wawekezaji wa kiafrika kuwekeza kwenye nchi yoyote bila kipingamizi.
Kamishina anayehusika na maendeleo ya viwanda kwenye umoja wa Afrika Albert Muchanga anasema kusainiwa na kutekelezwa kwa makubaliano hayo itakuwa ni hatua kubwa ambayo itawafaidisha wakazi wa bara la Afrika.
Balozi Muchanga anasema: "Hii ina maana kwamba sasa tunakwenda kulipanua soko letu…kilomita za mraba milioni 30 na wakazi zaidi ya bilioni moja nadhani hii ndiyo itakuwa ni sehemu kubwa ulimwenguni yenye soko la namna hii. Wakazi wa Afrika wengi ni vijana kwa wastani wa umri wa miaka 19, Afrika ina raslimali watu wenye nguvu za kutosha huo ni utajiri.Na hii itainua kiwango cha uwekezaji wa kimataifa niseme tu kwamba vijana sasa wamefata fursa kubwa."
Takwimu zinaonyesha mataifa ya Kiafrika yamekuwa yakifanya uwekezaji na biashara yenyewe kwa yenyewe kwa kiwango cha asilimia 15% huku uwekezaji baina ya Afrika na mabara mengine ukiwa zaidi ya asilimia 60%. Hali hii imetajwa kuwa sababu kubwa ya kulidhoofisha bara hilo kiuchumi.
No comments:
Post a Comment