Menaja wa Arsenal
Arsene Wenger amesema angependa sana Arsenal wasipangwe kukutana na
Atletico Madrid ya Uhispania katika ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa
League.
Hii ni baada ya Gunners kulaza AC Milan ya Italia 3-1 (Jumla 5-1) katika hatua ya 16 bora.Atletico Madrid wamekuwa wakicheza vizuri na walifika robofainali Europa League baada ya kuwalaza Lokomotiv Moscow 5-1 mechi ya marudiano.
Nyota wa zamani wa Liverpool na Chelsea Fernando Torres alifunga mabao mawili nao Angel Correa, Saul Niguez na Antoine Griezmann wakafunga moja kila mmoja Alhamisi na kuwawezesha Atletico kupata ushindi wa jumla wa 8-1.
- Tetesi za soka Ulaya Alhamisi 15.03.2018
- Chelsea yatupwa nje na Barca michuano ya UEFA
- Conte asema Chelsea kuchapwa 3-0 na Barcelona haikuwa haki
Mabao ya Arsenal yalifungwa na Danny Welbeck (mawili) na Granit Xhaka naye Hakan Calhanoglu akawafungia Milan bao la kufutia machozi Alhamisi.
"Bila shaka tungependa kuwakwepa Atletico Madrid," alisema Wenger.
Hata hivyo, alisema hana usemi wowote na wakikabidhiwa klabu hiyo hawatakuwa na budi ila kukutana nao.
Droo ya robofainali - ambapo kuna klabu nane kutoka mataifa manane - itafanyika leo Ijumaa saa 12:00 GMT.
Huu ulikuwa ushindi wa tatu wa Arsenal katika kipindi cha wiki moja baada ya kuwalaza Milan 2-0 mechi ya kwanza mjini Milan na pia wakalza Watford 3-0 Ligi ya Premia Jumapili.
Lakini kabla ya ushindi huo San Siro, walikuwa wameshindwa mechi nne mtawalia mashindano yote - mara mbili ikiwa mikononi mwa Manchester City.
"Mambo ni mazuri sana leo. Tulihitaji kujikwamua kutoka kwa matokeo yetu," Wenger alisema.
"Inaonesha jinsi timu ilivyochukua hatua. Tulikuwa na mechi ngumu lakini mwishowe tulishinda. Tukiwa na matokeo mazuri na jinsi tunavyocheza soka, mashabiki watatuunga mkono.
No comments:
Post a Comment